Kujiua

Kujiua
Mwainisho na taarifa za nje
SpecialtyPsychiatry, elimunafsia Edit this on Wikidata
ICD-10X60.X84.
ICD-9E950
MedlinePlus001554
eMedicinearticle/288598
MeSHF01.145.126.980.875

Kujiua (kwa Kiingereza "suicide" kutoka neno la Kilatini suicidium, lililotokana na sui caedere, "kujiua") ni kitendo cha mtu kujisababishia kifo kwa makusudi ama kwa kufanya kitu kinachoharibu uhai wake au kwa kuacha yale yanayohitajika kuuendeleza kama kula au kunywa.

Kuna sababu mbalimbali kwa nini watu wanajiua, kama vile

Mara nyingi, watu hujiua kufuatia hali ya kukata tamaa iliyosababishwa na tatizo la kiakili kama vile fadhaiko, maradhi ya hisia mseto, skizofrenia, ulevi au matumizi ya dawa za kulevya.[2]

Vipengele vya dhiki kama vile matatizo ya kifedha au matatizo katika mahusiano ya kijamii huchangia sana.

Juhudi za kuzuia kujiua hujumuisha kupunguza uwezekano wa kufikia bunduki, kutibu magonjwa ya akili, kuzuia matumizi mabaya ya dawa na kuboresha hali ya uchumi.

Mbinu za kujiua ni nyingi na upendeleo hutegemea mazingira na utamaduni. [3]. Inayotumika zaidi hutofautiana katika nchi mbalimbali na huhusishwa kwa kiasi na mbinu zinazopatikana. Mara nyingi hujumuisha: kujinyonga, kunywa sumu na kutumia bunduki.

Kwa jumla wanaume hutumia zaidi mbinu kali kama silaha au kujinyonga, wanawake njia ambazo ni pole zaidi kama kunywa sumu au kujizamisha kwenye maji.

Shirika la Afya Duniani linakadiria kwamba duniani kote kila baada ya sekunde 39 mtu mmoja anajiua, maana yake takriban watu 800,000 hadi milioni 1 hujiua kila mwaka.

Kwa hiyo tendo la kujiua ni kati ya sababu muhimu za kifo cha watu, ni kisababishi kikuu cha 10 cha vifo vyote ulimwenguni.[2][4] Idadi ya wanaume wanaojiua kwa jumla inazidi mara nne ile ya wanawake. Wazee hujiua kushinda vijana. [5][6]

Pamoja na wale wanaofaulu, kila mwaka kuna majaribio kati ya milioni 10 hadi 20[7]. Majaribio hayo mara nyingi huwa ya watoto na wanawake.

Waganga wa kisasa huona kujiua kama tatizo la afya ya nafsi; mara nyingi watu wanaojaribu kujiua hawataki kufa bali kuepukana na matatizo na kama wangeona njia ya kuachana na tatizo wasingejiua. Hivyo majaribio ya kujiua inaweza kuwa ya kuwaonyesha watu wa mazingira ya kwamba kuna tatizo zito na kuomba msaada.

Watu wanaorudia mara nyingi majaribio ya kujiua wanafaulu hatimaye kama hali yao haibadiliki.

Katika mafundisho ya dini nyingi tendo la kujiua linatazamwa kama dhambi au kosa.

Dini za Kiibrahimu zinachukulia kujiua kuwa dhambi kwa sababu ya imani juu ya utakatifu wa uhai, heshima na thamani ya maisha.

Katika Ulaya hadi karne ya 19 watu waliojiua hawakuzikwa makaburini pamoja na watu wengine lakini kando. Nchi mbalimbali zilikuwa na sheria dhidi ya wale waliojiua na jaribio lilitazamwa kama kosa la jinai.

Ingawa kosa la kujiua au kujaribu kujiua lilichangia adhabu ya kisheria hapo awali katika mataifa ya magharibi, kwa sasa haliadhibiwi. Kosa hili limesalia kuwa hatia katika mataifa mengi ya Kiislamu.

Kuna pia jamii ambako hatua ile inaheshimiwa kama azimio la kila mtu.

Katika utamaduni wa enzi za samurai nchini Japani kujiua kulitazamwa kama nafasi ya mkabaila kujirudishia heshima yake kama ameshindwa au kuonekana na kosa kubwa. Hivyo seppuku iliheshimiwa kama mbinu ya kulipia kosa la kushindwa au njia ya utetezi.

Katika utamaduni wa Uhindi mjane alisifiwa kama alijiua baada ya kifo cha mume wake hasa kwa kujichoma pamoja na maiti ya marehemu. Sati katika mazishi ya Kihindi, ambayo sasa imeharamishwa, ilimhitaji mjane kujitoa kafara kwa kujichoma katika kimbwi cha mazishi ya mumewe, kwa hiari au kwa kushinikizwa na familia na jamii.[8]

Katika karne ya 20 na 21, kujiua kwa mbinu ya kujitoa kafara kumetumika kama mbinu ya utetezi, na kamikaze na kujiua kwa bomu kama harakati za kijeshi au kigaidi.[9]

Hivyo katika vita vilivyopita askari walisifiwa kama waliamua kujiua kwa kutumia miili yao kama silaha dhidi ya adui. Mfano mashuhuri ni marubani wa kamikaze wa Japani waliojirusha pamoja na ndege zao dhidi ya meli za Marekani wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.

Wanamgambo wa Tamil Tiger nchini Sri Lanka walishambulia jeshi la serikali mara nyingi kwa mabomu hai yaani askari waliobeba bomu na kujilipua karibu na maadui.

Mbinu hiyohiyo inatumiwa pia katika dunia ya Kiislamu na wanamgambo na magaidi mbalimbali, hasa katika nchi kama Palestina, Irak au Afghanistan. Ilitumiwa pia na magaidi kutoka Checheniya dhidi ya Warusi.

  1. https://www.dailysignal.com/2022/06/13/study-connects-jump-in-youth-suicide-with-transgender-treatments-lack-of-parental-consent/?inf_contact_key=52c5d855ea18910d25fdd65d9dc7222b4dfbc39d7283b2cb89d5189540b69330
  2. 2.0 2.1 Hawton K, van Heeringen K (2009). "Suicide". Lancet. 373 (9672): 1372–81. doi:10.1016/S0140-6736(09)60372-X. PMID 19376453. {{cite journal}}: Unknown parameter |month= ignored (help)
  3. [http://www.who.int/bulletin/volumes/86/9/07-043489.pdf Methods of suicide: international suicide patterns derived from the WHO mortality database]
  4. Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; no text was provided for refs named Var2012
  5. Taarifa ya WHO
  6. Meier, Marshall B. Clinard, Robert F. (2008). Sociology of deviant behavior (toleo la 14th ed.). Belmont, CA: Wadsworth Cengage Learning. uk. 169. ISBN 978-0-495-81167-1. {{cite book}}: |edition= has extra text (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
  7. Bertolote JM, Fleischmann A (2002). "Suicide and psychiatric diagnosis: a worldwide perspective". World Psychiatry. 1 (3): 181–5. PMC 1489848. PMID 16946849. {{cite journal}}: Unknown parameter |month= ignored (help)
  8. "Indian woman commits sati suicide". Bbc.co.uk. 2002-08-07. Iliwekwa mnamo 2010-08-26.
  9. Aggarwal, N (2009). "Rethinking suicide bombing". Crisis. 30 (2): 94–7. doi:10.1027/0227-5910.30.2.94. PMID 19525169.

© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search